TUM YANILETEA UHALISIA WA NDOTO.

 


Mara nyingi watoto huwa na maono ya kuwa mtu au kitu fulani katika maisha. Jambo ambalo hukuzwa zaidi na mzazi au hata mwalimu pale shuleni. Ndiposa utamsikia mzazi au mwalimu akimuuliza mtoto angependa kuwa nani awapo mtu mzima. Ni jambo ambalo humwezesha mtoto kufahamu kwamba anao uwezo na nafasi ya kipekee kuwa yeyote atakaye maishani, bora bidii na imani.

Kama iwafanyikiavyo watoto wengine, haikua tofauti kwangu. Awali katika umri wangu mdogo, nilitamani sana kuwa daktari, wala si daktari tu bali daktari wa upasuaji. Hili lilitokana na kuwasikiliza watoto wenzangu waliotamani kuwa madaktari, nami nikawaiga. Sikutambua kwamba kila mtu aliumbwa na utofauti wa kipekee na kwamba maishani tungekuwa watu sawa lakini wanaojihusisha na mambo tofauti, nazungumzia wapo wangekua madaktari, walimu, wanahabari na mengineyo.

Jambo hili la mimi kuwa daktari liliendelea hadi nilipokuwa katika shule ya upili. Ndipo tulizungumziwa nikiwa kidoto cha pili wakati wa kuchagua masomo manane ambayo ningeendelea nayo hadi kidato cha nne. Ashukuriwe Mwenyezi Mungu kwa maana kutokana na mazungumzo yale, ndipo nilifahamu, nikapenda na kutamani kuwa mwanahabari.

Baada ya kuhitimisha kidato cha nne katika shule ya upili ya wavulana ya Bungoma, ndipo nilijiunga na chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa, almaarufu TUM. Hapo, nilijiunga kusomea kile nilichotamani na kuenzi, Uanahabari.

Baada ya kusajiliwa na kuwaa mwanafunzi wa chuo kikuu, jambo ambalo nilitamani sana tangia shule ya upili, changamoto za kutafuta nyumba ya kuishi zilianza. Awali, walionitangulia waliishi kunieleza kwamba maisha ya chuo kikuu ni matamu na yenye raha.

Naam, raha ipo, utamu wake pia upo, lakini walipaswa pia kutaja uchungu na changamoto zilizopo. Wakisema raha, niligundua walimaanisha uhuru uliopo vyuoni. Mtu anaweza kuhudhuria darasa atakavyo. Upo uhuru wa mavazi, ambao kwangu nilipenda sana. Niliishi kuchukia kuvalia sare ya shule, jambo ambalo lilichangia kufanya bidii kwangu ili nijipate ndani ya chuo kikuu.



Nilijiona mtu mzima wakati mzazi alinikodishia nyumba, akalala usiku mmoja na akaamkia kugura asubui yake. Kuachwa pekeyangu, nijue nala nini, napika ama nala hotelini, nitahudhuria darasa au nitalala, nitavaa kaptura au suruali ndefu niendapo darasani, nikichelewa darasani bado ninao uhuru na idhini ya ya kuingia bila ya kuulizwa swali na yeyote, ni matukio yaluonipendeza sana.

Hata hivyo, bali na uhuru huu wote, kugundua ndoto, maono na malengo niliokuwa nayo ndio yalinifanya kutofanya kinyume, licha ya uhuru huu. Nilihakikisha kwamba ninahudhuria darasa ipasavyo na kufanya ipasavyo ili angalau baada ya chuo niweze kuishi na kutimiza ndoto yangu ya kuwa mwanahabari.

Hata hivyo, baadhi ya changamoto nilizopitia ndani ya chuo, ni kuhudhuria darasa za asubui. Hii ilitokana na umbali nilioishi toka shuleni. Changamoto nyengine ilikua ni kujua nini ningepika. Sikupenda upishi sana, lakini kadri muda ulivyosanga ndivyo nilivyozidi kuzoea maisha ya chuo.



 Maisha ya chuo kikuu ni maisha ambayo kamwe sitoyasahau. Nilijifunza upishi mle, kuishi na watu wa tabaka mbalimbali, kuishi na wapangaji wenzangu tuliokodi nyumba pamoja, pamoja na mwenye nyumba, kujua kujifanyia mambo kivyangu kwa maana hakuna yeyote angekuja kufanya kwa niaba yangu, kama ilivyokuwa nyumbani na zaidi ya haya yote, chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa (TUM) kiliniwezesha kuafikia malengo na ndoto yangu ya kuwa mwanahabari.


                                           By Steve Kinyanjui. 

Comments

  1. Kazi safi kaka
    Napenda kazi yako pale studio pia

    ReplyDelete
  2. Kazi murwa kabisaπŸ”₯πŸ‘

    ReplyDelete

Post a Comment